Kutuma Ikisiri - CHAUKIDU 2026.
Kutuma au kufanyia tathmini ikisiri, utapaswa uwe na akaunti katika mfumo wetu wa ikisiri wa Kongamano la CHAUKIDU 2026. Ikiwa bado huna akaunti katika mfumo/tovuti yetu, tafadhali tengeneza akaunti kwa kutumia anuani-pepe yako na nywila utakayoichagua.
"Twen'zetu Makerere! Lulu ya Afrika Yaita. Upo?"
Mada Kuu
"Kiswahili na Lugha Nyingine Afrika: Mustakabali wa Ndani na Nje ya Mipaka ya Darasa katika Dunia Inayobadilika"
Kongamano hili linalenga kuwakutanisha watafiti, walimu, wanafunzi, watunga sera, wabunifu wa maudhui, na wadau mbalimbali kujadili nafasi ya Kiswahili katika dunia inayobadilika haraka. Ingawa Kiswahili kwa muda mrefu kimetazamwa kama lugha ya kufundishia darasani, kwa sasa kinapanuka katika matumizi halisi ya kijamii, kiuchumi, kidijitali, na kimataifa.
Katika muktadha wa utandawazi, maendeleo ya teknolojia, na mwingiliano wa lugha na tamaduni, kuna haja ya kuchunguza jinsi Kiswahili kinavyoweza kuendelea kuwa chombo hai cha mawasiliano, utambulisho, na maendeleo. Mkutano huu unatoa jukwaa la kubadilishana tafiti, uzoefu, na mbinu bunifu za kuendeleza Kiswahili nje ya darasa.
Dunia inabadilika kwa kasi kubwa. Utandawazi, mapinduzi ya dijitali, na mabadiliko ya kijamii na kiuchumi vinaendelea kuziathiri lugha zote. Kiswahili, pamoja na lugha nyingine zisemwazo na kufundishwa barani Afrika na kwingineko, zinaguswa moja kwa moja na mabadiliko hayo, huku umadhubuti wa sera, utoshelevu wa rasilimali, na uhai wa lugha nyingi vikiendelea kutikiswa.
CHAUKIDU inawaalika watafiti, walimu, wataalamu wa teknolojia, watunga sera, wadau mbalimbali, na wasemaji wote wanaojali mustakabali wa lugha katika zama hizi kushiriki katika mjadala utakaofanyika katika Kongamano la 10 la Kimataifa la Kiswahili. Tunalenga kubadilishana maarifa, kujadili matokeo ya tafiti, na kupanga mikakati ya kuimarisha matumizi, ufundishaji, na maendeleo ya lugha hizi katika zama hizi za mabadiliko.
Mada kuu ya kongamano hili ni Kiswahili na Lugha Nyingine Afrika: Mustakabali wa Ndani na Nje ya Mipaka ya Darasa katika Dunia Inayobadilika.
Kamati ya maandalizi inakaribisha ikisiri zinazoangazia maeneo mbalimbali yakiwemo: ufundishaji na ujifunzaji wa Kiswahili na lugha za Kiafrika; teknolojia na Akili Ige (AI); lugha za Kiafrika katika elimu ya awali, sekondari, na ya juu; matumizi ya lugha nje ya darasa; lugha za Kiafrika katika vyombo vya habari, biashara, na diplomasia; tafsiri, ukalimani, na maendeleo ya istilahi; sera za lugha na upangaji lugha; uhifadhi na uendelezaji wa lugha zilizo hatarini; fasihi, utamaduni, na utambulisho katika ulimwengu wa kisasa; lugha za Kiafrika katika diaspora na mawasiliano ya kimataifa; na ujasiriamali wa lugha na uchumi wa lugha.
Unakaribishwa kuwasilisha ikisiri ya maneno 200 - 250, ukibainisha wazi mada, lengo kuu, mbinu, na mchango unaotarajiwa. Ikisiri zote ziandikwe kwa kuzingatia mojawapo ya mada ndogo zilizoorodheshwa hapo chini, huku zikiwianishwa na mada kuu ya kongamano.
Mada Ndogo za Uwasilishaji
Chagua mada ndogo inayoendana na utafiti wako wakati wa kuwasilisha ikisiri.
Mwongozo wa Uwasilishaji
- Kichwa cha ikisiri kiwe kinaeleweka vizuri: Kisipungue maneno matano na kisizidi maneno 20. Kisiwe na istilahi za kiujumla sana (mf. Kiswahili na TEHAMA). Kiwe kinaendana na maudhui ya wasilisho yaliyobainishwa katika ikisiri
- Maudhui ya ikisiri: Maudhui ya ikisiri ndiyo hasa kiini cha tathmini. Maudhui yawe na maneno yasiyozidi 200 na yawe yanagusia mada kuu na moja ya mada ndogondogo za kongamano hili. Sehemu kubwa ya maamuzi ya tathmini itajiegemeza katika kipengele hiki. Utapewa sehemu ya kuchagua mada ndogo inayoendana na wasilisho/ikisiri yako.
- Lugha ya Uandishi: Mwandishi atumie lugha fasaha na inayokubalika katika muktadha wa kitaaluma. Ikisiri isiwe na makosa ya kitahajia na iwe na mtiririko mzuri wa mawazo.
- Mwandishi anaweza kuwasilisha ikisiri ya zaidi ya watu (mmoja awe mwandishi wa kwanza).
- Usiandike Majina Yako: Tathmini zitafanyika katika mfumo wa 'double blind'. Mtathmini hapaswi kujua jina la mwandishi wa ikisiri anayoitathmini. Hivyo, katika ikisiri hiyo, usiandike majina yako popote. Ukishajisajili kwenye mfumo, tutajua ikisiri hiyo imetumwa nawe, ila usiweke majina kwenye ikisiri yenyewe, au kwenye kichwa.anuani ya ikisiri. Kama utaweka kiambatisho chochote, usiandike majina humo pia.
Makundi ya Uwasilishaji
Mchakato wa Kutathmini Ikisiri
- 1Kutuma/kuwasilisha IkisiriWaandishi kutuma ikisiri kupitia kwa mfumo.
- 2Tathmini na UhaririKutathmini ikisiri kuzingatioa mada kuu na ndogo, upeo na mpangilio.
- 3Kuhitimisha tathmini za ikisiriWahariri wawili huru; wa tatu kwa kufungua sare.
- 4TaarifaMaamuzi yatatangazwa ifikapo tarehe 30 Septemba 2026.
Tuma ikisiri yako kupitia mfumo wetu wa mwito wa ikisiri. Ikiwa wewe ni mgeni, utahitaji kuunda akaunti yako kwanza.
