Kuhusu CHAUKIDU
Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani — daraja linalounganisha wapenzi wa lugha, utamaduni, na elimu katika mabara yote.
Malengo ya CHAUKIDU
Kutangaza lugha ya Kiswahili maeneo yote duniani na kuongeza mahusiano kati ya maeneo hayo na Afrika Mashariki, lugha ya Kiswahili na utamaduni wa Waswahili. Vilevile, chama kina malengo ya kuwaunganisha wadau wa Kiswahili waliotawanyika kwenye pembe nne za dunia.
Madhumuni yetu ya Msingi
Kukuza Kiswahili katika nyanja zote ambamo lugha hii inatumika au inaweza kutumika na kuongeza ufanisi wa mawasiliano katika ufundishaji na utafiti wa maarifa ya aina zote, uandishi/utangazaji wa habari, uandishi wa vitabu, uchapishaji vitabu na majarida, utayarishaji wa safari za mafunzo katika Afrika ya Mashariki na Kati, n.k.
Kuwaunganisha wanachama wote kwa malengo ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika maswala mbalimbali yahusianayo na Kiswahili (mfano. mbinu za ufundishaji, utangazaji, utafiti, uandishi n.k.) kwa kuratibu makongamano ya kila mwaka, washa, makongamano maalumu, na makongamano ya mitandaoni.
Kuuelimisha umma kuhusu umuhimu wa kujivunia kuwa Mswahili, kuendeleza na kuitangaza fahari ya Kiswahili.
Kuzishauri na kuzihimiza serikali za nchi ambazo Kiswahili huzungumzwa kuitambua thamani ya Kiswahili ili kufanya yote yawezekanayo katika kuunda sera madhubuti ambazo zitahakikisha maendeleo ya Kiswahili kijamii, kisiasa na kiuchumi, na kuuendeleza utamaduni wa watu wake.
Historia ya CHAUKIDU
Chama hiki, CHAUKIDU, kimeanzishwa baada ya miaka mingi ya kuomba, maandalizi, na mijadala mingi miongoni mwa wapenzi wa Kiswahili kutoka maeneo mbalimbali duniani, ambao wote walikuwa na hamu ya kuona uanzishwaji wa jumuiya ya watu watakaokuwa tayari kujitoa mhanga kwa kushirikiana na taasisi na jumuiya nyingine kukiendeleza na kukitangaza Kiswahili katika nyanja zote ili kukiletea heshima ndani na nje ya Afrika. CHAUKIDU kilizinduliwa na katiba yake kupitishwa katika mkutano uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Wiskonsin mnamo tarehe 26 Aprili, 2012.
Kwa mujibu wa katiba yake, Makao Makuu ya CHAUKIDU kwa sasa yako katika Chuo Kikuu cha Georgia, nchini Marekani, ambako Rais wa sasa huishi na kufanya kazi, hadi hapo atakapostaafu au awamu yake itakapokwisha. Chama kilianzishwa kikiwa na malengo ya kuhimiza na kuharakisha maendeleo ya Kiswahili duniani kote.
Kuwa Mwanachama
Jiunge na CHAUKIDU kuunga mkono fani hii na kupata punguzo la viwango vya kongamano mwaka mzima.
Ni Kwanini Ushiriki?
Yawezekana unajiuliza swali hili: ni kwanini nishiriki kwenye kongamano hili? Nitapata faida gani?
Jumuiya ya Kimataifa
Wasomi kutoka nchi mbalimbali! Kongamano la Kimataifa la CHAUKIDU linakuwa fursa ya kujumuika katika harakati za kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili.
Wasemaji Mahiri
Kongamano hili litakupa fursa ya kusikiliza mawasilisho ya mada elekezi kutoka kwa wasemaji mahiri na waliobobea katika fani zao.
Ajenda ya Kiafrika
Kongamano hili linakupa fursa ya kukutana na watu mbalimbali toka sehemu mbalimbali za dunia. Ushirikiano na vyuo vikuu, serikali na asasi zisizo za kiserikali.
