Kiswahili na Lugha Nyingine za Kiafrika katika Zama za AI: Fursa na Changamoto
Katika zama hizi za Akili Mnemba/Akili Unde (Artificial Intelligence – AI), ambapo teknolojia hii inaendelea kubadilisha kila nyanja ya maisha ya binadamu, uga wa lugha haujaachwa nyuma. Kwa hakika, hata msingi wenyewe wa mifumo ya AI ni lugha. AI imechochea kasi ya matumizi, uenezaji, na utafiti wa lugha katika viwango vipya kabisa. Teknolojia hii imefungua milango ya fursa lukuki kwa walimu, wanafunzi, watafiti, na watumiaji wa lugha katika nyanja mbalimbali. Hata hivyo, pamoja na fursa hizo, zipo pia changamoto mbalimbali zinazojitokeza ama katika uundwaji wa mifumo yenyewe, au katika matumizi ya mifumo hiyo. Katika muktadha huo, maswali na mijadala inaendelea kuibuka kuhusu namna ambavyo fursa na changamoto hizo zinaigusa lugha ya Kiswahili na lugha nyingine za Kiafrika. Ikiwa teknolojia hizi zimebuniwa na kuendelezwa zaidi katika mataifa na lugha kubwa za Kimagharibi, Bara la Afrika na lugha zake zinawekwa katika nafasi gani? Je, ni kwa kiasi gani uchakataji wa lugha ya Kiswahili na lugha nyingine za Kiafrika katika mifumo ya AI unazingatia ufasaha, usanifu, kaida, na tamaduni za lugha hizo? Je, AI inaleta fursa na changamoto gani ambazo watafiti, walimu, wasemaji, watunga sera, na wadau wengine wa Kiswahili na lugha nyingine za Kiafrika wanapaswa kuzizingatia?
CHAUKIDU inafikiri ni vyema kuwa na mjadala wa kina katika suala hili, na kongamano letu la Kimataifa ndilo litupalo uwanja mpana wa kufanya hivyo kwa mafanikio makubwa. Wanachama wa CHAUKIDU na wadau wote wa Kiswahili na teknolojia wanakaribishwa kutuma ikisiri za makala zinazochambua ama kujadili suala hili katika kongamano la 10 la Kimataifa la CHAUKIDU. Wanaweza kutuma ikisiri za makala kuhusu mada kuu ya Kongamano huku wakimakinikia mada ndogondogo zifuatazo:
- AI, Teknolojia, na Ukuzaji wa Kiswahili
- AI na Isimu/Isimu Tumizi ya Kiswahili
- AI na Hali ya Kiswahili Nyumbani na Ughaibuni
- AI na Ufundishaji wa Kiswahili kwa Wageni
- AI na Tafsiri/Ukalimani
- AI na Usanifu/Ufasaha wa Kiswahili
- AI, Uundaji wa Istihali, na Utengenezaji Kamusi
- AI, Maadili, Utamaduni, na Maarifa ya Kiasili
- AI na Lugha ya Kufundishia
- AI, Fasihi, na Sanaa ya Kiswahili
- AI na Uhifadhi wa Lugha za Kiasili
- AI na Lugha Nyingine za Kiafrika
- AI na Ushindani wa Kiswahili dhidi ya Lugha Nyingine Kuu
- Kiswahili, AI na Utafiti na Uchapishaji
- Kiswahili, AI, na Mitandao ya Kijamii
- Kiswahili, AI, na Uanaharakati
- Kiswahili, AI, na Uchumi
- Kiswahili, AI, Siasa, Utangamano, na Diplomasia
- Kiswahili, AI, na Usalama wa Mtandaoni
- Kiswahili, AI, Uhuru wa Kiteknolojia, na Umajumui wa Afrika
- Mada nyengine itakayopendekezwa na mwandishi wa makala (mada-pendekezwa izingatie mada kuu)
